Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama latoa tamko kuhusu unyanyasaji wa kingono CAR

Baraza la Usalama latoa tamko kuhusu unyanyasaji wa kingono CAR

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo wametoa taarifa wakieleza kutiwa hasira na madai ya unyanyasaji wa kingono uliofanywa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Hii ni kufuatia hotuba ya Katibu Mkuu wa Baraza hilo mnamo Agosti 13, ambapo alielezea hatua zilizochukuliwa na Umoja wa Mataifa, ikiwemo kumwachisha Mwakilishi wake Maalum, Babacar Gaye kazi.

Katika taarifa, Wajumbe wa Baraza la Usalama wamesema walinzi wa amani wanapaswa kuwalinda raia katika maeneo walikopelekwa, na kwamba walinda amani wa Umoja wa Mataifa hawana budi kutimiza vipengele vya sheria ya kimataifa, ikiwemo inayohusu kuheshimu haki za binadamu.

Aidha, wamesema Umoja wa Mataifa usiwaache watu wachache watie doa kazi ya ujasiri ya makumi ya walinda amani na wahudumu wa Umoja wa Mataifa, wakikaribisha kujitoa kwa Katibu Mkuu kutekeleza sera ya kutovumilia kabisa vitendo vya ukiukaji sheria, pamoja na mapendekezo yake za kuhakikisha ujumbe wote wa kulinda amani unatimiza sera hiyo.

Wamekumbusha pia wajibu wa nchi zinazochangia walinda amani kuchunguza madai dhidi ya askari wao na kuwashtaki pale inapohitajika na kuufahamisha Umoja wa Mataifa kuhusu harakati hizo za kisheria.