Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha kusainiwa kwa makubaliano ya amani Sudan Kusini

Ban akaribisha kusainiwa kwa makubaliano ya amani Sudan Kusini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataia, Ban Ki-moon, amekaribisha kusainiwa kwa mkataba wa amani baina ya aliyekuwa Makamu wa Rais Sudan Kusini, Riek Machar na Watu waliokuwa wamezuiliwa zamani, hapo jana Jumatatu.

Taarifa ya msemaji wake inasema kuwa Katibu Mkuu anafahamu pia kuwa Rais Salva Kiir aliweka herufi za jina lake kwenye nakala ya mkataba huo akionyesha kutoridhika. Kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu ameelezea matumaini yake makubwa kuwa Rais Kiir atausaini mkataba huo kabla siku 15 kwisha.

Bwana Ban ametoa shukrani kwa upatanishi wa IGAD, na kwa juhudi zake za kusaidia pande kinzani kufikia makubaliano, na kuelezea kutiwa moyo na uungaji mkono wa makubaliano hayo kwa ngazi za kikanda na kimataifa.

Taarifa hiyo pia imesema kuwa Katibu Mkuu anatiwa uchungu na kuteseka kwa raia wa Sudan Kusini, na kutoa wito kwa pande kinzani kusitisha uhasama mara moja, na kudumisha sheria ya kimataifa ya haki za binadamu na sheria ya kibinadamu. Aidha, amezitaka kushirikiana na UNMISS na wahudumu wa kibinadamu katika jitihada za kuokoa maisha nchini Sudan Kusini.