Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR na wadau kusaidia Libya kuokoa maisha baharini

UNHCR na wadau kusaidia Libya kuokoa maisha baharini

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na maswala ya wakimbizi, UNHCR limeshiriki katika kuweka jukwaa la kusaidia Libya katika kujibu wito kwenye pwani yake kwa kuimarisha usambazaji wa taarifa na uratibu wa mashirika ya kimataifa. Lengo ni kuimarisha uwezo wa kuokoa maisha baharini na kusaidia katika kukusanya maiti ya wanaopoteza maisha, pamoja na kuiimarisha huduma kwa manusura wa ajali za boti.

Taarifa za UNHCR zinasema kwamba Shirika hilo linatambua umuhimu wake miongoni mwa wadau mbali mbali, likiongeza kuwa mafunzo yatakayotolewa kwa kundi hilo yatajumuisha kuuliza maswali kwa manusura kabla hawajahamishwa kutoka walikowekwa, kwa ajili ya kubaini idadi ya wanaowasili na kituo wanakopelekwa kwa ajili ya utaratibu wa kuwaachia hususan wanawake na watoto.

Leo Dobbs ni msemaji wa UNHCR Geneva,

“Kundi hili la wataalamu litajadili mbinu za kupunguza vifo miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji ambao wanajaribu kuvuka bahari ya Mediterenia na watakutana mara tatu kwa kipindi cha miezi tisa ijayo.”

Kundi hilo litajumuisha maafisa kutoka walinzi wa pwani ya Libya, mamlaka ya kuzuia uhamiaji haramu, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM na  UNHCR.