Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili miungano ya kikanda na changamoto za kiusalama

Baraza la Usalama lajadili miungano ya kikanda na changamoto za kiusalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekutana kujadili uimarishaji wa amani na usalama wa kimataifa, likimulika hasa miungano ya kikanda na changamoto za kisasa kwa usalama wa kimataifa.

Akihutubu katika kikao cha leo, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema Umoja wa Mataifa unazidi kugawana wajibu wa kudumisha amani na usalama na miungano ya kikanda. Kwa mantiki hiyo, amesema Umoja wa Mataifa unapaswa kufanya kila liwezekanalo kuisaidia miungano hiyo kuyatatu matatizo yao ya kikanda, na kushirikisha nchi husika.

Akizungumza kuhusu ubia kati ya Umoja wa Mataifa na miungano ya kikanda, Ban amesisitiza haja ya kushirikiana na Muungano wa Afrika, ili kuimarisha viwango wastani vya utendaji kazi, na kuboresha uhamishaji wa mamlaka kutoka vikosi vya AU kwenda kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Uratibu zaidi wa utaratibu na kushauriana kuhusu sera, mwongozo na viwango vya mafunzo utasaidia kutimiza viwango vya utendaji kazi kwa ngazi zote. Haki za binadamu ni lazima zipewe kipaumbele. Maoni yetu yanaweza kutofautiana wakati mwingine, lakini tukiendelea kupigania amani, usalama na haki za binadamu, tutasalia kwenye mkondo wa kufikia mustakhbali salama zaidi.”

Ban amesema viongozi ni lazima watambue kuwa amani itaepusha majanga ya kibinadamu na kuchochea maendeleo ya kiuchumi, na kuongeza kuwa ni lazima kuweka matarajio ya hali ya juu kwa nchi husika, na kuzisaidia kufikia ustawi wa kudumu.