Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM, AMISOM, IGAD, EU na Uingereza watoa heko kwa uchaguzi Jubba, Somalia

UM, AMISOM, IGAD, EU na Uingereza watoa heko kwa uchaguzi Jubba, Somalia

Wadau wa kimataifa nchini Somalia wamepongeza kuchaguliwa kwa Sheikh Ahmed Mohamed Islam “Madobe” na Baraza la mkoa mnamo Agosti 15, kuwa rais wa serikali ya mpito ya jimbo la Jubba.

Katika taarifa ya pamoja, wadau hao, wakiwa ni Umoja wa Mataifa, Ujumbe wa Afrika Somalia, AMISOM, IGAD, Muungano wa Ulaya, EU na Uingereza wamepongeza ahadi ya Sheikh Madobe ya kushirikiana kwa dhati na kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu Omar Abdirashid Ali Sharmarke ili kushughulikia suala la uwakilishi kwenye Baraza la Mkoa, na kumsihi achukue hatua za kulitatua suala hilo hima ma kwa njia jumuishi.

Wamekaribisha pia uungaji wake mkono wa matokeo ya jukwaa la ngazi ya juu la ubia, pamoja na azimio la Baraza la Usalama namba 2232(2015).

Wamesema wadau ndani ya Somalia wataendelea kuchagiza rasilmali kupitia utaratibu uliopo, kwa minajili ya kutoa huduma muhimu kwa raia na kuimarisha uwezo wa serikali ya mpito ya jimbo la Jubba.