Skip to main content

Ni mchakato jumuishi wa kisiasa tu ndilo suluhu kwa mzozo wa Syria- Baraza la Usalama

Ni mchakato jumuishi wa kisiasa tu ndilo suluhu kwa mzozo wa Syria- Baraza la Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limesisitiza leo kuwa suluhu endelevu pekee kwa mzozo wa Syria sasa ni kupitia mchakato wa kisiasa ulio jumuishi, na ambao unatimiza matarajio ya watu wa Syria kwa kutekeleza azimio la Geneva la Juni 30 2012. Kwa mantiki hiyo, Baraza la Usalama limesisitiza haja ya pande zote kuchukua hatua za dharura na kufanya bidii ili kutimiza dhamira hiyo.

Katika taarifa ya rais wake, Baraza hilo limekariri pia wito lililotoa katika azimio namba 2139, kwamba pande kinzani zikomeshe mara moja mashambulizi dhidi ya raia, pamoja na matumizi ya silaha kiholela katika maeneo ya raia wengi, yakiwemo mabomu.

Aidha, limekariri wito wa kukomesha kuwazuilia watu kiholela, utesaji, utekaji nyara, ukiwemo wa wanahabari na wahudumu wa kibinadamu, na kutaka wito huo utekelezwe kulingana na sheria ya kimataifa.

Halikadhalika, Baraza la Usalama limeeleza kusikitishwa na baadhi ya maeneo ya Syria kuwa chini ya makundi ya kigaidi kama vile ISIL na Al Nusrah Front, na kulaani vitendo vingi vya kigaidi vinavyoendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kupitishwa taarifa hiyo na Baraza la Usalama, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa, Alexis Lamek ametaja aina nne za ujumbe unaowakilishwa katika taarifa hiyo, ukiwemo kuungana kwa Baraza la Usalama, ujumbe wa kisiasa kuhusu ugaidi na haja ya kutimiza matakwa ya watu wa Syria.

Ujumbe wa tatu ni wa kulaani. Baada ya mashambulizi yaliyofanywa Damascus siku chache zilizopita, baraza linakariri kuwa mashambulizi ya kioholela dhidi ya raia ni lazima yakomeshwe. Na ujumbe wa nne ni wa kuunga mkono Stafan de Mistura. Stafan de Mistura amejaribu kufufua tena mchakato wa kisiasa, kazi yake ikiwa ni kuongoza utekelezaji wa azimio la Geneva la Juni 2012. Sasa ana uungwaji mkono wa dhati wa Baraza la Usalama”