Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asikitishwa na kuongezeka machafuko mashariki mwa Ukraine

Ban asikitishwa na kuongezeka machafuko mashariki mwa Ukraine

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameeleza kusikitishwa na kuongezeka kwa machafuko hivi karibuni mashariki mwa Ukraine, ambayo yameripotiwa kusababisha vifo vya raia kwenye pande zote za makabiliano.

Taarifa kutoka ofisi ya msemaji wake imesema kuwa Katibu Mkuu anafahamu ripoti za kusumbuliwa kwa ujumbe maalum wa Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya (OSCE) unaofuatilia hali ya mambo nchini Ukraine, na kwamba anatarajia pande zote kuheshimu jukumu la OSCE, maafisa wake na vifaakazi vyao.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande zote pia kuendelea na mazungumzo na kutimiza moyo wa makubaliano ya Minsk, ikiwemo kuhusu matumizi ya silaha nzito.  Ametoa wito pia kwa pande kinzani kuchukua hatua za kurejesha utulivu, na kuzuia wimbi la ghasia ambalo litsababisha vifo zaidi, maafa kwa binadamu na uharibifu wa miundombinu, pamoja na kuvuruga ustawi wa kikanda.

Ametoa wito pia wahudumu wa kibinadamu wawezeshwe kuwafikia wenye mahitaji ya dharura, na kuwezesha uhuru wa kutembea kwa raia kote nchini.