Wenye uhitaji Syria wawezeshwe kutafuta uslama na misaada – Mkuu wa OCHA

17 Agosti 2015

Mratibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura katika Umoja wa Mataifa, Stephen O’Brien, amekamilisha ziara ya siku tatu Syria leo, akionya kuwa mgogoro wa muda mrefu nchini humo hauathiri tu maisha ya mamilioni ya watu, lakini pia unatishia ustawi wa ukanda mzima na zaidi.

Katika ziara hiyo, Bwana O’Brien alitembelea mji wa Homs, ambako aliweza kujionea madhara ya mapigano, na kukutana na familia ambazo hivi karibuni zimerejea kwenye mji huo.

Bwana O’Brien ameeleza kusikitishwa na ripoti za mashambulizi ya angani hapo jana katikati mwa mtaa wa Douma, mjini Damscus, ambayo yaliwaua makumi ya raia na kuwajeruhi mamia ya wengine. Amesema mashambulizi dhidi ya raia ni kinyume na sheria, hayakubaliki na ni lazima yakomeshwe.

Akizungumza kuhusu kukatizwa huduma za maji kwa jumla ya watu milioni saba katika miji ya Damacus na Aleppo, Bwana O’Brien ameongeza kuwa haikubaliki pia kukatiza huduma za maji kwa raia kama silaha ya vita.

Katika kipindi cha zaidi ya miaka minne ya mzozo huo, zaidi ya watu 220,000 wameuawa, zaidi ya milioni moja kujeruhiwa na takriban nusu ya raia wote wa Syria kulazimika kuhama makwao.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter