Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon ataka ushiriki katika kupambana na “saratani” ya ubakaji

Ban Ki-moon ataka ushiriki katika kupambana na “saratani” ya ubakaji

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekuwa na mkutano wa faragha na wanachama wa Baraza la Usalama kuhusu visa vya ubakaji vinavyodaiwa kuwa vimetekelezwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa waliopo Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bwana Ban amesema visa hivi ni saratani kwa Umoja wa Mataifa, akisikitishwa na kuona kwamba bado visa vingi haviripotiwi, na hivyo havipelekwi mahakamani na sheria haitekelezwi.

Katibu Mkuu amezingatia uwajibikaji wa kila mmoja katika kukabiliana na tatizo hilo, kuanzia mtu binafsi hadi viongozi, pia Umoja wa Mataifa wenyewe na nchi wanachama. Amesema swala la uwajibikaji ndilo lililomsababisha kumwomba Babacar Gaye, ambaye alikuwa mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa CAR, kujiuzulu.

Amesema kwamba tayari Umoja wa Mataifa umejitahidi kuimarisha ufuatiliaji katika idara ya ulinzi wa amani ili kuwa na uwezo wa kubaini visa vya ukatili wa kingono na kuchukua hatua haraka, huku akieleza kwamba maswala ya maadili na nidhamu yamesisitizwa zaidi.

Hatimaye ametangaza kumteua Parfait Onanga-Anyanga kuwa Kaimu Mwakilishi wake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wakati huo. Bwana Onanga-Anyanga amekuwa mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi hadi Disemba mwaka 2014.