UNAIDS yamulika wanawake wenye ukimwi wanaozaa watoto bila ukimwi Afrika Mashariki
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maswala ya ukimwi UNAIDS limezindua kitabu kipya kinachoonyesha hadithi ya akina mama 12 wanaoishi na virusi vya ukimwi, lakini wamefanikiwa kuzaa watoto ambao hawakuambukizwa virusi vya ukimwi. Taarifa kamili na Grace Kaneiya
(Taarifa Grace)
Lengo la kitabu hiki kinachoitwa Sura za kizazi bila ukimwi Afrika Mashariki na Kusini, ni kuhamasisha jamii kuhusu huduma za kuzuia maambukizwi ya ukimwi kutoka kwa mama hadi mtoto wakati wa ujauzito na miaka ya kwanza ya mtoto.
Kwa mujibu wa UNAIDS, idadi ya wanawake wanaopata huduma za kuzuia maambukizi haya imeongezeka sana kwa kipindi cha miaka michache iliyopita, na kufika asilimia 88 ya wanawake wajawazito wanaoishi na ukimwi kwenye ukanda huo.
UNAIDS imesema kuwa matokeo yake ni kupungua kwa asilimia 60 kwa maambukizi ya watoto kutoka kwa mama kati ya mwaka 2009 na 2014.
Hata hivyo bado ni theluthi moja tu ya watoto wanaoishi na ukimwi kwenye ukanda wa Afrika mashariki na kusini ndio wanapata matibabu, na takwimu zinaonyesha kwamba bila matibabu wengi wao hawataweza kufikisha umri wa miaka mitano.