Ukwepaji sheria Burundi unachochea machafuko zaidi- UM

14 Agosti 2015

Ofisi ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, imetoa wito kwa serikali ya Burundi ichukue hatua za kuwalinda raia na kufanya uchunguzi katika vitendo vya uhalifu ili wakiukaji wa haki za binadamu wawajibishwe.Taarifa kamili na Joseph Msami.

(Taarifa Msami)

Ofisi hiyo imesema hali ya haki za binadamu nchini Burundi imeendelea kuzorota, huku watu 96 wakiwa wameuawa, hususan kutoka upande wa upinzani, tangu machafuko yanayohusiana na uchanguzi yalipoanza mwishoni mwa mwezi Aprili.

Watu wapatao 600 walikamatwa katika kipindi hicho, ingawa wengi wao wameachiwa huru. Kumekuwa na visa vipatavyo 60 vya utesaji na vitendo vingine vya kutaabisha katika vituo vya polisi na idara ya ujasusi. Ravina Shamdasani ni msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu, Geneva

“Idadi kamili ya watu waliouawa, kuwekwa kizuizini au kuteswa huenda ikawa juu zaidi. Tunatoa wito kwa serikali kuchukua hatua kuwalinda wanaharakati wa mashirika ya kiraia na wanahabari. Machafuko yanayoendelea nchini humo yameathiri vibaya kufurahia kwa haki nyingi za binadamu.”

Ofisi hiyo imesema Burundi imeendelea kufuata mkondo hatari kwa mauaji ya watu maarufu, na kutoa wito kwa viongozi wa pande zote kuchukua hatua za kupinga ghasia na kutatua tofauti zao kwa njia ya amani.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter