Ban ajadili ukatili wa kingono na wakuu wa ulinzi wa amani

13 Agosti 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameongea leo na wakuu wa operesheni za ulinzi wa amani na makamishna wa polisi kupitia njia ya video kuhusu tatizo la ukatili wa kingono lililotokea Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kwenye mkutano huo wa dharura Bwana Ban amesisitiza umuhimu wa kutostahimili visa hivyo na tabia yoyote isiyoheshimu maadili ya Umoja wa Mataifa.

Akiongea na waandishi wa habari baada ya mkutano huo mjini New York, Marekani, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema kuwa Katibu Mkuu amezingatia jukumu la viongozi wa operesheni za ulinzi wa amani katika kupambana na tabia mbaya na ukatili wa kingono,

“ Amesema pia kwamba wakuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wanawajibika moja kwa moja kwa kuhakikisha tabia nzuri na nidhamu kwenye ujumbe wao. Amewaomba viongozi wa operesheni za ulinzi wa amani kutumia fursa zote za kukariri ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kukataa aina yoyote ya tabia mbaya ikiwemo ukatili wa kingono.”

Hatimaye ameziomba nchi zinazochangia walinda amani kuhakikisha kwamba wanajeshi wao wamefundishwa ipasavyo kuhusu tabia nzuri na nidhamu.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter