Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMI yalaani vikali mashambulizi ya bomu Baghdad

UNAMI yalaani vikali mashambulizi ya bomu Baghdad

Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Kaimu Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, UNAMI, Gyorgy Busztin, amelaani vikali mashambulizi  ya bomu ya gari ambayo yalifanyika katika soko la Jameela katika mji wa Sadr, Baghdad Mashariki na kuwaua angalau watu 45 huku wengine wengi wakijeruhiwa. Idadi hii inatarajiwa kuongezeka. Ripoti zinasema kwamba kundi linalotaka kuweka dola la Uislamu wenye itikadi kali, ISIL limedai kutekeleza mashambulizi hayo.

Mkuu huyo wa UNAMI amelaani vikali mashambulizi hayo ambayo yanalenga raia wasio na hatia wakiwemo watoto katika soko la umma.

Ameongeza kwamba shambulizi hilo la kiholela linalenga kudhoofisha mshikamano wa watu wa Iraq, huku akiongeza kwamba ana uhakika kwamba magaidi hao hawatafaulu.

Bwana Busztin ametuma salamu zake kwa wahanga na familia zao na kuwatakia afueni ya haraka majeruhi, huku akiongeza kwamba ni lazima wahusika wafikishwe katika vyombo vya sheria.