WFP yaanza kusambaza pesa kwa msaada wa chakula Ukraine

13 Agosti 2015

Shirika la Mpango wa Chakula WFP limeanza kutoa msaada wa fedha kwa watu karibu 60,000, hasa wakimbizi wa ndani, kwenye maeneo ya Lugansk na Donetsk mashariki mwa Ukraine.

Katika taarifa iliyotolewa leo, mwakilishi wa WFP nchini Ukraine Giancarlo Stopponi amesema vocha za pesa zinatumiwa kwenye maeneo ambapo bado benki na masoko yanafanya kazi ili kuwezesha watu kununua vyakula wanavyopenda.

Bwana Stopponi ameongeza kuwa vocha hizo pia zinaingiza pesa kwenye uchumi wa maeneo hayo na kuendeleza biashara sokoni.

Mradi huo wa WFP unalenga takriban watu 140,000, kila mmoja akipatiwa msaada wa dola 20.50 kwa mwezi kwa ajili ya kununua chakula. Kwa ujumla ni watu zaidi ya 500,000 wanaosaidiwa na WFP.

Kwa mujibu wa WFP, watu milioni 5 wameathirika na mzozo unaoendelea nchini Ukraine, wakiwemo watoto milioni 1.7.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter