Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mvutano wa kisiasa unahatarisha demokrasia Guinea Bissau- Baraza la Usalama

Mvutano wa kisiasa unahatarisha demokrasia Guinea Bissau- Baraza la Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na mjadala wa faragha kuhusu mzozo unaoendelea nchini Guinea-Bissau, baada ya rais Jose Mario Vaz kuifuta serikali yake kufuatia mvutano na Waziri Mkuu Domingos Pereira.

Kwenye taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo, wanachama wa baraza hilo wamesema mvutano kati ya rais na waziri mkuu unahatarisha mafanikio yaliyokuwa yamepatikana baada ya kurejeshwa kwa utawala wa sheria mwaka 2014 kufuatia uchaguzi mkuu. Aidha wamesisitiza umuhimu wa utaratibu wa maridhiano, utawala bora na udhibiti wa serikali kupitia mamlaka za kiraia ili kudumisha amani nchini humo.

Akihojiwa na Redio ya Umoja wa Mataifa, Mkuu wa Ujumbe wa Amani na mwakilishi wa Katibu Mkuu nchini humo Miguel Trovoada amekariri wito huo.

(Sauti ya Trovoada)

“ Jamii ya kimataifa inatoa wito kwa mamlaka za serikali kutafuta suluhu kupitia njia ya mazungumzo na maelewano ili kulinda amani na utulivu nchini humo na kutatua mvutano uliozidi, ambao umesababisha matokeo tunayoshuhudia sasa”