Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola yamulikwa Baraza la Usalama likikutana kuhusu amani na usalama Afrika

Ebola yamulikwa Baraza la Usalama likikutana kuhusu amani na usalama Afrika

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekutana kuhusu amani na usalama barani Afrika, likimulika hasa jitihada za kimataifa dhidi ya mlipuko wa homa ya kirusi cha Ebola mwaka 2013.

Baraza hilo limehutubiwa kwa njia ya video na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Margaret Chan akiwa Hong Kong, na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Ebola, Dkt. David Nabarro, akiwa Geneva.

Katika hotuba yake, Dkt. Margaret Chan amesisitiza umuhimu wa hatua zimepigwa katika kukabiliana na Ebola, Guinea na Sierra Leone zikiwa zimeripoti visa vitatu tu katika wiki mbili zilizopita, lakini akaonya

“Wakati huo huo, ni lazima nionye kuhusu kulegeza umakini. Inachukua kisa kimoja kisichogundulika katika kituo cha afya, mtu mmoja aliyeambukizwa kutoroka kutoka mfumo wa ufuatiliaji, au kisa kimoja cha mazishi yasiyo salama kuibua tena visa vingi vya Ebola.”

Naye Dkt. Nabarro amesisitiza umuhimu wa kuhusisha jamii katika jitihada za kukabiliana na mlipuko

“Hofu ya watu inakabiliwa kwa urahisi, tamaduni muhimu zinafanywa kuwa salama na kuheshimiwa, mitandao ya maambukizi inagundulika haraka, waliokaribiana na wagonjwa wanatambuliwa haraka na mlipuko unamalizika haraka zaidi, iwapo jamii zinahusishwa katika jitihada.”