Skip to main content

Baraza la Usalama kukutana Alhamis kuhusu walinda amani na unyanyasaji wa kingono

Baraza la Usalama kukutana Alhamis kuhusu walinda amani na unyanyasaji wa kingono

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ametangaza leo kuwa amemwomba rais wa Baraza la Usalama kuitisha kikao maalum hapo kesho kujadili suala unyanyasaji wa kingono miongoni mwa vikosi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Ban ametoa tangazo hilo wakati akikutana na waandishi wa habari, ambapo pia ametangaza kujiuzulu kwa mwakilishi wake maalum na mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA, Babacar Gaye.

Aidha, Katibu Mkuu amesema kuwa kesho Alhamis ataitisha mkutano kwa njia ya video wawakilishi wake maalum, makamanda wa vikosi vya wanajeshi na makamishna wa polisi katika operesheni zote za ulinzi wa amani ili kusisitiza wajibu wao.

Nitakariri kuwa viongozi ni lazima waripoti madai mara moja, wachunguze kikamilifu na kuchukua hatua mathubuti. Kushindwa kufanya hivyo kutakuwa na matokeo ya wazi. Nitaendelea kutoa shinikizo ili juhudi zaidi zifanywe. Ninataka viongozi wajue kwamba wanawajibika kwa vikosi vyao, polisi na raia. Wanapaswa pia kuhakikisha kuwa wote wanaendelea kupata elimu na mafunzo ya haki za binadamu.”

Ban ametoa wito pia kwa nchi wanachama zishiriki katika jitihada za kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji wa kingono miongoni mwa askari wao walinda amani.

Nataka wahalifu wajue kwamba wakitenda uhalifu, tutafanya kila liwezekanalo kuwaandama na kuwapeleka mbele ya sheria. Nataka waathiriwa wajue kwamba tutajitahidi kutimiza wajibu wetu kitaasisi kulinda usalama na utu wao. Kwa waathiriwa, nasema, tunasimama nanyi. Tafadhali jitokezeni. Msione aibu. Aibu ni kwa wanaotenda uhalifu"