Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban atangaza kujiuzulu kwa mkuu wa MINUSCA, Babacar Gaye

Ban atangaza kujiuzulu kwa mkuu wa MINUSCA, Babacar Gaye

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ametangaza leo kujiuzulu kwa Mwakilishi wake maalum, na Mkuu wa Ujumbe wa kurejesha utulivu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA Babacar Gaye, kufuatia ujumbe huo kughubikwa na madai ya unyanyasaji wa kingono.

Katibu Mkuu amesema anaamini kuwa kiwango cha madai ya unyanysaji wa kingono, ambayo yameonekana katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kabla na baada ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa kupelekwa huko, kinaonyesha haja ya kuchukua hatua sasa.

“Na itoshe sasa. Leo nimekubali kujiuzulu kwa Mwakilishi wangu maalum Babacar Gaye, Mkuu wa Ujumbe wa pamoja wa kuweka utulivu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA. Ninapofanya hivyo, ningependa kuenzi juhudi zake katika kutumikia amani, usalama na maridhiano katika kipindi kirefu cha kuhudumu kwake, hususan katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, katika mazingira magumu, wakati wa mzozo ambao haujawahi kushuhudiwa.”

Ban amesema unyanyasaji wa kingono ni janga la kimataifa na changamoto ya kimfumo inayohitaji kukabiliwa kimfumo.