Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Unyanyasaji wa kingono hauwezi kukubalika katika Umoja wa Mataifa – Ban

Unyanyasaji wa kingono hauwezi kukubalika katika Umoja wa Mataifa – Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema leo kuwa unyanyasaji wa kingono daima hauwezi kukubaliwa, hususan katika Umoja wa Mataifa, ambao unapigania haki za wanawake na watoto duniani.

Akikutana na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Ban amesema wanawake na watoto hawapaswi kufanywa kuwa waathiriwa mara mbili kwa kukosa haki

“Siwezi kueleza jinsi nilivyokerwa, kukasirishwa na kuaibishwa ripoti za mara kwa mara kwa miaka mingi, za unyanyasaji wa kingono unaofanywa na vikosi vya Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa unapopeleka walinda amani, unafanya hivyo kuwalinda watu walio hatarini zaidi duniani katika maeneo yenye taabu zaidi. Sitovumilia kitendo chochote ambacho kinaifanya imani ya watu kuwa uoga.”

Ban amesema wafanya kazi wa Umoja wa Mataifa ni lazima waonyeshe maadili ya viwango vya juu zaidi. Amesema madai yote ya unyanyasaji wa kingono yanapaswa kuchunguzwa kikamilifu, kwani vitendo vya aibu vya watu wachache vinaweza kudunisha kazi ya ujasiri ya makumi ya maelfu ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa.

“Mjuavyo, nimeteua jopo huru la ngazi ya juu kuchunguza kwa karibu ripoti za unyanyasaji wa kingono katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na tunavyokabiliana nayo katika mfumo wetu. Natazamia kupokea matokeo ya uchunguzi wao.”