Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana wanaweza kusaidia kutimiza malengo ya maendeleo endelevu- Ban

Vijana wanaweza kusaidia kutimiza malengo ya maendeleo endelevu- Ban

Ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya Vijana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema leo kuwa vijana wa sasa wanaweza kusaidia katika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, baada ya serikali kuafikia malengo hayo ya mwaka 2030 wiki iliyopita. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Akihutubu katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani kwenye Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu amesema vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo umaskini, migogoro na ukosefu wa ajira.

Hata hivyo, Bwana Ban amesema vijana hawakubali tu changamoto hizo kama hatma yao.

“Wanathubutu kupinga mifumo ya uongozi, wakipaazia sauti haki, na haki za binadamu, na wanachagiza hatua za kimataifa kwa maslahi ya wanadamu na sayari dunia. Tunapoadhimisha siku hii kwa kauli mbiu ya kushirikisha raia, nashikamana na wanaharakati hawa vijana.”

Katibu Mkuu amesema malengo ya maendeleo endelevu ni kwa ajili ya vijana, na yanaweza tu kutimizwa na vijana.

Ajenda mpya inalenga kumaliza umaskini. Inachukua sura ya kina, ikijumuisha maendeleo ya mazingira, kijamii na kiuchumi.Katika kutekeleza ajenda hii, nategemea vijana duniani kuwa wabeba mwenge wa maendeleo endelevu.”