Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana wapaaze sauti, na viongozi wasikilize- Ban

Vijana wapaaze sauti, na viongozi wasikilize- Ban

Ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya Vijana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito kwa vijana wapaaze sauti na kuzungumzia changamoto zinazowakabili, na kwa viongozi wawasikilize vijana hao.

Katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku hii, Ban ametaja baadhi ya changamoto zinazowakabili vijana sasa kama matishio mapya, itikadi kali na katili, mabadiliko ya mazingira ya kisiasa mizozo ya kiuchumi na mabadiliko ya kijamii.

Ban amesema hakuna anayefahamu changamoto zinazowakabili vijana kama vijana wenyewe, wala jinsi ya kukabiliana nazo.

Amesema ulimwengu unapobadilika kasi, vijana wanaonekana kuwa wadau wanaoweza kuchangia masuluhu muhimu, akipongeza mamilioni ya vijana ambao wanaandamana kupigania haki na kushirikishwa, kukabiliana na viwango vya juu vya ukosefu wa ajira, kupigania haki na kuchagiza hatua za kimataifa kwa maslahi ya wanadamu na sayari dunia.