Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zapigwa katika kuwalinda watoto Sudan Kusini dhidi ya kipindupindu

Hatua zapigwa katika kuwalinda watoto Sudan Kusini dhidi ya kipindupindu

Idadi ya visa vya kipindupindu imeanza kupungua nchini Sudan Kusini kufuatia jitihada za Shirika la Afya Duniani, WHO na wadau wake, ambao wanaendelea kupambana na mlipuko wa ugonjwa huo kwa matibabu ya kuokoa maisha kwa maelfu ya watu.

Kampeni za afya zinazooanishwa na utamaduni na imani za wenyeji zimesaidia kuendeleza mienendo ya usafi kama vile kunawa mikono kwa sabuni, usafi katika kuandaa vyakula na kuvihifadhi na katika unyonyeshaji watoto.

Hata hivyo, mlipuko huo unaendelea kuwa tishio kubwa kwa watoto na makundi mengine yaliyo hatarini nchini Sudan Kusini, mathalan waja wazito, wazee na wenye mahitaji maalum, kama vile watu wanaoishi na HIV na magonjwa sugu.

Kufikia Agosti 10, jumla ya visa 1519 vilikuwa vimeripotiwa tangu mwezi Juni, huku watoto wenye umri chini ya miaka mitano, na kati ya miaka mitano na tisa wakiathiriwa zaidi katika majimbo ya Juba na Bor.