Mtaalam wa UM asihi Brazil isiwafurushe watu wa asili

Mtaalam wa UM asihi Brazil isiwafurushe watu wa asili

Mtalaam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya watu wa asili Victoria Tauli-Corpuz ameisihi leo serikali ya Brazil kuheshimu haki za binadamu za watu wa jamii za Guarani na Kaiowá.

Amesema hayo baada ya kueleza wasiwasi wake kuhusu ripoti kwamba polisi ya Brazil inafukuza watu hao wa asili kutoka kwa ardhi yao asilia, kwenye mkoa wa Mato Groso do Sul, mashariki mwa nchi, akisema anahofia usalama wao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya haki za binadamu, bado watu wa asili 6,000 wamekata kufukuzwa kwa ardhi yao iitawyo “Tekohas” wakisema watapinga mpango huo hadi kufa kwao.

Akitaja Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Watu wa Asili, mtalaam huyo ameeleza kwamba watu wa asili hawapaswi kufukuzwa kwa ardhi yao kama hawajakubali na kupewa sehemu nyingine ya kuishi inayolingana na ile ya awali.

Ofisi ya Haki za Binadamu imesema tangu miaka ya 1920 watu wa asili wananyanyaswa na kufukuzwa kwa ardhi yao kwa ajili ya kukuza kilimo cha biashara nchini Brazil. Tangu 2003, zaidi ya watu 290 wa jamii za Guarani na Kaiowá wameuawa kutokana na mvutano huo.