Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fumbua macho kuhusu taabu ya raia wa Yemen- rais wa ICRC

Fumbua macho kuhusu taabu ya raia wa Yemen- rais wa ICRC

Rais wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu ICRC Peter Maurer amesema dunia inapaswa kufumbua macho kuhusu mateso ya raia nchini Yemen.

Amesema hayo baada ya kutimiza ziara ya siku tatu nchini humo, ambapo alitembelea maeneo ya Aden na Sana’a yaliyoathiriwa na mzozo, na kukutana na viongozi.

Akiongea kwenye ujumbe wa video uliochapishwa kwenye tovuti ya ICRC baada ya kutembelea hospitali ya Mansoura iliyopo mjini Aden, Bwana Maurer amesema matokeo ya mapigano na vizuizi dhidi ya uingizaji bidhaa yameathiri sana sekta ya afya.

“ Nimeona watu ambao wamejeruhiwa vibaya. Nilipoingia hospitalini, hakukuwa na mtu kwenye kitengo cha dharura. Baada ya nusu saa, niliporudi, wagonjwa wawili walikuwepo, wakiwa wameathirika sana na mabomu na mabomu ya kutegwa ardhini. Ni janga linaloenea hapa Aden, na mengi zaidi yanapaswa kufanywa ili kusaidia wahanga wanaoteseka kila siku na mzozo huo.”

Takwimu za ICRC zinakadiria kwamba watu 4,000 wameuawa tangu mwanzo wa mzozo, huku wengine 19,000 wakijeruhiwa.

Rais wa ICRC ameomba uingazaji na usafirishaji wa bidhaa ndani ya nchi urahisishwe, pamoja na usambazaji wa misaada ya kibinadamu.