Umoja wa Mataifa watoa ufadhili wa mara moja kwa raia wa CAR

11 Agosti 2015

Umoja wa Mataifa umetoa dola milioni 13 kwa ajili ya kusambaza mara moja msaada wa kibinadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Maswala ya Kibinadamu OCHA limesema ufadhili huo utasaidia mashirika ya kibinadamu kutoa huduma za maji safi, afya, elimu, chakula na makazi kwa wakimbizi wa ndani, wakimbizi na watu wengine walioathirika na mzozo.

Hata hivyo, pesa hizo zilizotolewa na Mfuko wa Pamoja wa Kibinadamu nchini CAR, CHF ni asilimia 3 tu za dola milioni 415 zinazohitajika kwa ajili ya kutimiza mahitaji ya raia wa CAR.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, bado watu 450,000 ni wakimbizi wa ndani nchini humo, huku milioni 2.7 wakihitaji msaada wa kibinadamu wa dharura.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter