Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upeni fursa mchakato wa amani Libya- Bernardino Leon

Upeni fursa mchakato wa amani Libya- Bernardino Leon

Mazungumzo yanayolenga kurejesha amani nchini Libya yameng’oa nanga leo mjini Geneva, huku Mpatanishi mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bernardino Leon akitoa wito kwa pande husika kutoa fursa ya ufanisi kwa mazungumzo hayo.

Bwana Leon ameutoa wito huo mjini Geneva akikutana na waandishi habari, akiongeza kuwa anatarajia kuzileta pande kinzani pamoja kwa maslahi ya watu wa Libya.

Leon amesema lengo ni kuwezesha pande zote kufikia makubaliano mapema mwezi Septemba ili kumaliza miaka minne ya mgogoro tangu kupinduliwa kwa serikali ya Muammar Gaddafi

Bwana Leon amesema dhamira ya mazungumzo ya Geneva ni kujadili masuala yanayohusu pande zote na kuweka serikali ya pamoja.

“Kwa hiyo tutaendelea kusikiliza, tutaendelea kufanya kazi nao wote, na tunatumai kuwa watatoa fursa kwa mchakato huu, na itawezekana kuendelea kufanya kazi ili kuona hatma ya yote mwisho wa siku.”

Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto nyingi zinazokabili kufikia makubaliano, na kwamba kufikia makubaliano hakutategemea kushughulikia masuala ya upande mmoja tu.