UM wasikitishwa na kuachiliwa kwa washukiwa wa uhalifu wa vita Mali

UM wasikitishwa na kuachiliwa kwa washukiwa wa uhalifu wa vita Mali

Ofisi ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, imeeleza kusikitishwa na kuachiliwa huru kwa watu waliokuwa wamezuiliwa nchini Mali wakishukiwa kuhusika katika vitendo vya uhalifu mbaya mno, ukiwemo uhalifu wa kivita, vitendo vya kigaidi na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Ofisi hiyo imesema inafahamu kuwa baada ya kuachiliwa watu hao mnamo Julai 16 mwaka huu, huenda wengine wataachiliwa hivi karibuni.

Imeongeza kuwa hatua yoyote ambayo itaonekana kama msamaha itakuwa inakiuka sheria ya kimataifa, na kwenda kinyume na ahadi za pande husika za makubaliano ya amani na maridhiano. Ravina Shamdasani ni msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu, Geneva

“Tunasisitiza umuhimu wa kupambana na ukwepaji sheria na haja ya kuchunguza na kufungua mashtaka dhidi ya ukiukaji wote wa haki za binadamu ili kuwe na uwajibikaji.”

Bi Shamdasani amesema utoaji msamaha unaozuia kushtakiwa kwa watu ambao huenda wamehusika katika uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhkiukaji wa haki za binadamu ni kinyume na wajibu wa serikali chini ya mikataba ya sheria ya kimataifa.