Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma za afya nchini Yemen zazidi kudhoofika, WHO yahitaji ufadhili

Huduma za afya nchini Yemen zazidi kudhoofika, WHO yahitaji ufadhili

Mfumo wa afya nchini Yemen unazidi kudhoofika, raia wakikosa huduma muhimu za kuokoa maisha.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani WHO, tayari asilimia 23 ya vituo vya afya nchini humo vimefungwa kutokana na mapigano, vingine vikitarajia kufungwa kadri ghasia inavyoendelea.

Sababu nyingine ni ukosefu wa umeme na mafuta yanayohitajika kuendesha  vitengo vya magonjwa mahututi, pia kukimbia nchi kwa wataalam wa afya na madaktari wengi.

WHO imesaidia wizara ya afya ya Yemen kwa kutoa msaada wa tani 181 za vifaa mbalimbali, pamoja na kusambaza timu 70 za madaktari na wauguzi, na mafuta zaidi ya lita 700,000.

Hata hivyo bado ukata wa fedha unalikumba shirika hilo, dola milioni 130 bado zikihitajika ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Tarik Jasarevic ni msemaji wa WHO, Geneva

"Iwapo hatutapokea ufadhili huu katika muda wa miezi michache ijayo, huduma muhimu za afya zitalazimika kukatizwa ikiwemo huduma kwa watu walio na kiwewe na huduma za upasuaji, huduma msingi ya afya, afya ya waja wazito, uchunguzi wa magonjwa na huduma ya kukabiliana na magonjwa."