Ban ataka iendelezwe afya na maslahi ya watu wa asili kupitia ajenda 2030

10 Agosti 2015

Azimio kuhusu haki za watu wa asili limesaidia kuboresha maisha ya kundi hilo tangu lipitishwe na Baraza Kuu mnamo mwaka 2007, lakini bado kuna mengi ya kufanya, hasa katika mwaka huu yanapowekwa malengo ya maendeleo endelevu.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, akihutubia leo mkutano uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Watu wa Asili.

Katibu Mkuu amesema, ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu ni mpango mathubuti wa kuchukua hatua kutokomeza umaskini, akiongeza kuwa hakuna mtu anayepaswa kuachwa nyuma, hususan watu wa asili

“Wao ni miongoni mwa watu walio hatarini zaidi duniani, na waliotelekezwa zaidi, licha ya kwamba historia yao, utamaduni wao, lugha na maarifa ni sehemu ya msingi wa urithi wa wanadamu. Watu wa asili wanaweza kuufundisha ulimwengu kuhusu mienendo endelevu ya maisha na kuhusiana vyema na mazingira.”

Katibu Mkuu amesema siku hii inamulika kuendeleza afya na maslahi ya watu wa asili kupitia ajenda ya maendeleo ya 2030.

“Watu wa asili wana haki ya kufurahia viwango vya juu zaidi vinavyoweza kupatikana vya afya ya mwili na akili. Hiyo inamaanisha kupata huduma zote za kijamii na afya. Na inamaanisha kutunza haki ya kuendelea na mifumo ya kijadi ya afya na Imani. Watu wa asili wanakabiliwa na changamoto nyingi kiafya na hali, na nyingi zinazuilika”

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kama kutokuwa na huduma za kutosha za kujisafi, makazi, huduma za waja wazito na ukatili ulioenea dhidi ya wanawake.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter