Mkakati wa Israel wa kupanua makazi yake ni msingi wa ghasia Palestina: wataalam wa UM

Mkakati wa Israel wa kupanua makazi yake ni msingi wa ghasia Palestina: wataalam wa UM

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya kuchunguza vitendo vya Israel vinavyoathiri haki za binadamu kwenye maeneo ya Palestina yaliyotawaliwa imetimiza leo tathmini yake ya kila mwaka ikisema mkakati wa Israel wa kuendelea kujenga makazi kwenye maeneo mapya ni msingi unaochochea ghasia kwenye maeneo hayo.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo baada ya ziara yake ya siku tano nchini Jordan, kamati hiyo maalum imesema mkakati huo unaoendelea na ukwepaji sheria huchangia kwa kiasi kikubwa kwenye vurugu inayozidi kwenye maeneo ya Palestina yaliyotawaliwa.

Juu ya hayo, visa vya ukiukaji wa haki za binadamu vimeongezeka kwa mujibu wa kamati, ikieleza kuwa wanawake na watoto huathirika na uchunguzi unaofanywa usiku na wanajeshi wa Israel na mbwa wao.

Halikadhalika, kamati imemulika ukata wa fedha unaolikumba Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi wa Palestina, UNRWA, huku ikieleza kwamba bado wakazi wa Gaza wamekosa sehemu ya kuishi, na watu 120,000 hawajarejeshewa huduma za maji.