Umoja wa Mataifa wataka haki ya watu wa asili ya kupata huduma za afya izingatiwe

Umoja wa Mataifa wataka haki ya watu wa asili ya kupata huduma za afya izingatiwe

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameeleza matumaini yake ya kuimarisha maisha ya watu wa asili kupitia ajenda mpya ya maendeleo endelevu ya baada ya mwaka 2015, akisema kwama lengo lake ni kuhakikisha hakuna mtu mmoja aliyeachwa nyuma katika hali ya umaskini.

Amesema hayo leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya watu wa asili, mwaka huu maudhui yake yakiwa ni maswala ya afya na kijamii.

Kwenye ujumbe wake kwa siku hiyo, Bwana Ban amesema bado watu wa asili wanakumbwa na changamoto kadhaa kwa upande wa afya, ikiwa ni ukosefu wa huduma za afya ya uzazi, ukatili wa kijinsia, kiwango cha juu cha visa vya ugonjwa wa sukari na matumizi ya madawa ya kulevya na pombe, akieleza kwamba matatizo hayo mengi yanazuilika.

Halikadhalika amesisitiza umuhimu kwa watu wa asili kutunza ujuzi wao wa kyenyeji kuhusu maswala a afya, aidha kuhakikisha kwamba wanaweza kupatiwa huduma zote za afya na kijamii za kisasa.