Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusirudie Nagasaki wala Hiroshima, aomba Ban Ki-moon

Tusirudie Nagasaki wala Hiroshima, aomba Ban Ki-moon

Leo ikiwa ni miaka 70 baada ya bomu la nyuklia kulipuka mjini Nagasaki nchini Japan, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema shambulio hilo linapaswa kuwa la mwisho kihistoria, kwa sababu matokeo yake kwa maisha ya binadamu ni makubwa mno.

Kwenye ujumbe wake uliosomwa kwa niaba yake na Kim Won-soo, ambaye ni Kaimu Mwakilishi Mkuu kuhusu masuala ya uondoaji silaha, wakati wa kumbukizi iliyofanyika leo, Katibu Mkuu amepongeza jitihada za makazi na viongozi wa Nagasaki katika kusambaza wito huo wa kutokomeza silaha za nyuklia duniani kote.

Aidha amepongeza pia bidii za manusura waitwao Hibakusha ambao nao wamechangia katika kupitisha ujumbe huo wa amani, akiongeza kwamba ni lazima urithi wao na ujumbe wao udumu wakati ambao wengi wao wanafikisha umri wa miaka 80 na zaidi.

Hatimaye amekariri msimamo wa Umoja wa Mataifa wa kuhamasisha dunia nzima ili kuondoa hatari ya nyuklia.