Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lalaani shambulio la kigaidi Saudia Arabia

Baraza la Usalama lalaani shambulio la kigaidi Saudia Arabia

Wanachama wa Baraza la Usalama wamelaani vikali shambulio la kigaidi lililotokea tarehe 6 Agosti nchini Saudia Arabia kwenye msikiti uliokuwa karibu na makao makuu ya jeshi, mkoani Asir, karibu ya mpaka wa Yemen, ambapo watu wapatao 15 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Wanachama hao wamesema kundi linalotaka kuweka dola la Uislamu wenye itikadi kali, ISIL, lililodai shambulio hilo linapaswa kuangamizwa na chuki linalosambaza inapaswa kukomeshwa.

Aidha wanachama wa baraza hilo wametuma salamu zao za rambirambi kwa familia za wahanga na serikali ya Saudia.

Wamekariri msimamo wao wa kupambana na wafuasi wa kundi hilo na vikundi vingine vya kigaidi, wakisisitiza umuhimu wa kupeleka watekelezaji wa uhalifu huo mbele ya sheria.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amelaani pia shambulio hilo, akisema kuwa hakuna misingi yoyote inayoweza kufanya likubaliwe. Msemaji wake Stephane Dujarric amewaeleza waandishi wa habari ujumbe wa Katibu Mkuu

"Anatumai kuwa wahalifu watakabiliwa kisheria. Katibu Mkuu anatuma rambi rambi zake kwa familia za wahanga, kwa serikali na watu wa Ufalme wa Saudia. Anawatakia majeruhi nafuu haraka."