Ban atoa tamko kuhusu machafuko maeneo ya Palestina yaliyokaliwa

Ban atoa tamko kuhusu machafuko maeneo ya Palestina yaliyokaliwa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amelaani mashambulizi mengi ya roketi zilizorushwa Israel kutoka Gaza katika siku chache zilizopita.

Taarifa ya msemaji wake imesema Katibu Mkuu ameeleza pia kutiwa wasiwasi na machafuko ya hivi karibuni katika maeneo yaliyokaliwa ya Ukingo wa Magharibi, Jerusalem Mashariki na Gaza.

Machafuko hayo yanajumuisha pia shambulizi la kugonga kwa gari hapo jana karibu na eneo la makazi la Shiloh, ambalo lilisababisha majeraha kwa wanajeshi wawili wa Israel, bomu la moto ambalo lilimjeruhi vibaya mwanamke Muisraeli hapo Jumatatu Agosti 3 na machafuko ya umwagaji damu baada ya shambulio la kigaidi la Duma, ambalo lililaaniwa kimataifa, ikiwemo na Israel.

Katibu Mkuu amelaani vitendo hivyo, akitarajia kuwa pande zote zitavilaani na kuzuia vitendo kama hivyo. Ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa na kijamii wa Israel na Palestina kutoruhusu watu wenye msimamo mkali kuzorotesha hali na kunyakua udhibiti wa ajenda ya kisiasa.