Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laidhinisha wabainishwe waliotumia silaha za kemikali Syria

Baraza la Usalama laidhinisha wabainishwe waliotumia silaha za kemikali Syria

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo kwa kauli moja wamepitisha azimio la kutaka uwekwe utaratibu wa kuchunguza na kuwatambulisha watu, makundi au serikali ambazo zilihusika katika matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Wakilaani vikali matumizi ya kemikali zenye sumu kali kama vile gesi ya klorini kama silaha ya vita nchini Syria, wajumbe wa Baraza la Usalama wamekariri azimio lao la kuipinga Syria kuunda, kuagiza, kuhifadhi silaha za kemikali.

Wamekariri pia kuwa hakuna upande wowote nchini Syria unaopaswa kuunda, kuzalisha, kuhifadhi au kutumia silaha za kemikali, huku wakielezea ari yao kuwatambua wale waliohusika katika matumizi ya silaha za kemikali.

Kwa mantiki hiyo, wamemwomba Katibu Mkuu ashirikiane na Shirika la Kupinga Matumizi ya Silaha za kemikali, OPCW, kuwasilisha kwa baraza hilo mapendekezo ya utaratibu wa uchunguzi wa pamoja wa wahusika wa matumizi ya silaha hizo katika kipindi cha siku 20.

Wajumbe wametoa maelezo baada ya kupitisha azimio hilo, mmoja wao akiwa ni Samantha Power, Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani

(Sauti ya Samantha Power)

“Azimio la leo limepitishwa kwa kauli moja ya Baraza hili. Hili linatuma ujumbe bayana na wenye nguvu kwa wote waliohusika katika mashambulizi ya silaha za kemikali Syria. Utaratibu wa pamoja wa uchunguzi utakutambulisha ukiwashambulia watu kwa gesi. Ni vyema kurudia pia kuwa, tunapaswa kuleta umoja tulioonyesha leo, ili kupata haraka suluhu la kisiasa kwa mzozo wa Syria.”