Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP kupunguza msaada wa chakula kwa wakimbizi wa Syria waliopo Kurdistan

WFP kupunguza msaada wa chakula kwa wakimbizi wa Syria waliopo Kurdistan

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP limetangaza leo kupunguza msaada wake kwa baadhi ya wakimbizi wa Syria waliopo kwenye ukanda wa Kurdistan nchini Iraq baada ya kuhitimisha tathmini kuhusu upatikanaji wa chakula kwenye eneo hilo.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, WFP imesema kuwa uhaba wa chakula siyo tatizo kubwa linalokumba zaidi wakimbizi wa Syria waliopo kambini nchini Iraq, kwani nchi hii inawaruhusu kuajiriwa na hivyo kulipwa mshahara na kusaidia familia zao. Asilimia 85 ya wakimbizi wa Syria nchini Iraq wanapata riziki kutoka ajira na biashara mbalimbali, imesema taarifa.

Kutokana na tathmini hiyo, WFP imeamua kupunguza hadi dola kumi kwa mwezi vocha za msaada wa chakula kwa zaidi ya watu 47,000, huku ikitangaza kulenga watu 1,000 wanaoteseka zaidi kwenye eneo hilo na kuendelea kuwapa vocha za dola 19 kwa mwezi.

Aidha wakimbizi 50,000 waliokuwa wakipewa msaada wa WFP hawatapewa tena msaada wa chakula.

Kwa ujumla, ni wakimbizi wa Syria milioni 1.6 kwenye nchi tano za ukanda huo ambao wanapewa vocha za chakula kila mwezi.