Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban wakimbizi 400 wanusuriwa baada ya boti kuzama pwani ya Libya

Takriban wakimbizi 400 wanusuriwa baada ya boti kuzama pwani ya Libya

Watu wapaato 400 wamenusuriwa kufikia sasa kutoka kwa chombo kilichozama kwenye pwani ya Libya wakijaribu kuvuka Bahari ya Mediterenia, ikikadiriwa kuwa chombo hicho kilikuwa kimewabeba watu wakimbizi na wahamiaji wapatao 600.

Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, ambalo limesema pia kuwa miili ya watu 25 imeokolewa, lakini wengine wengi bado hajulikani walipo, wakihofiwa kufariki dunia katika janga hilo la Jumatano Agosti 5.

Kabla ya janga hilo, watu wapatao 2,100 wamefariki dunia mwaka huu wakijaribu kuvuka Bahari ya Mediterenia kwenda Ulaya.

Akisema kuwa  wakimbizi na wahamiaji hawastahili kufariki wakitafuta maisha bora, Msemaji wa UNHCR, Melissa Fleming, amesema manusura wameelezea jinsi boti yao ilivyokuwa imejazwa watu kupita uwezo wake, na jinsi watu walivyoshikwa na uoga walipoona chombo cha uokozi kikikaribia, na hivyo kukimbilia upande mmoja na kuifanya boti yao iegemee upande na kupinduka.