Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 70 baada ya mabomu ya kiatomoki ya Hiroshima na Nagasaki, waathirika bado wanatibiwa: ICRC

Miaka 70 baada ya mabomu ya kiatomoki ya Hiroshima na Nagasaki, waathirika bado wanatibiwa: ICRC

Leo ikiwa ni miaka sabini baada ya mabomu ya atomiki kulipuka kwenye miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan, bado maelfu ya manusura wanatibiwa kutokana na athari zake za muda mrefu.

Taarifa iliyotolewa leo na Shirika la kimataifa la msalaba mwekundu ICRC inasema kwamba theluthi mbili ya vifo vya manusura vimesababishwa na saratani.

Mkuu wa ICRC Peter Maurer amesema athari hizo zinaonyesha umuhimu wa kutokomeza matumizi ya silaha za nyuklia.

Tangu kufunguliwa kwa hospitali za Shirika la Msalaba mwekundu mijini Hiroshima na  Nagasaki mwaka 1956 na 1969,  zaidi ya manusura milioni 5 wametibiwa humo.

Kumbukizi ya miaka 70 ya mabomu ya nyuklia inafanyika miezi michache baada ya mkutano wa tathmini ya mkataba wa kudhibiti matumizi ya silaha za nyuklia (Non-Proliferation of Nuclear Weapons) kushindwa kukubaliana kuhusu mwelekeo ili kutokomeza silaha hizo.