Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulaya ndiyo yenye viwango vya chini zaidi vya kunyonyesha watoto- WHO

Ulaya ndiyo yenye viwango vya chini zaidi vya kunyonyesha watoto- WHO

Bara la Ulaya ndilo lenye viwango vya chini zaidi vya unyonyeshaji wa watoto, kwa mujibu wa Shirka la Afya Duniani, WHO.

WHO imesema, kati ya mwaka 2006 na 2012, ni asilimia 25 tu ya watoto wachanga ndio walionyonyeshwa tu kwa miezi sita ya kwanza katika ukanda wa Ulaya, ikilinganishwa na asilimia 43 katika ukanda wa Kusini- Mashariki mwa Asia.

Kulingana na WHO, unyonyeshaji watoto ndiyo njia bora zaidi ya kuwalisha watoto wachanga, na kwamba kufanya hivyo kunahakikisha watoto wanakuwa vyema, na kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza baadaye maishani.

Unyonyeshaji unapaswa kuwa ndiyo njia pekee ya kuwalisha watoto katika miezi sita ya kwanza ya maisha, na unachukuliwa kama moja ya vitendo muhimu zaidi vya kuendeleza na kulinda afya.

WHO imesema, mitazamo bora kuhusu waja wazito, ushirikiano wa heshima unaowajumuisha wanawake katika kufanya uamuzi wakati wa uja uzito na uzazi, na huduma bora za afya ni muhimu katika afya ya wazazi na watoto katika ukanda wa Ulaya.