Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya kuimarika kwa hali ya usalama CAR, bado msaada wa kimataifa wahitajika

Licha ya kuimarika kwa hali ya usalama CAR, bado msaada wa kimataifa wahitajika

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana leo kujadili hali ya usalama na ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, siku tatu baada ya kuuwawa kwa mlinda amani mmoja . Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Akizungumza mbele ya Baraza la Usalama, mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini CAR MINUSCA, Babacar Gaye amesema mwelekeo nchini humo ni mzuri kwa sababu ya mafanikio ya kisiasa na kurejeshwa kwa hali ya usalama hasa mjini Bangui, hatua iliyowezesha baadhi ya wakimbizi wa ndani kurudi makwao.

Hata hivyo ameeleza kwamba bado maeneo kadhaa ya nchi yanakumbwa na vurugu kutokana na uhalifu wa waasi wa Ex-Seleka na LRA, na mvutano wa kikabila.

Aidha bwana Gaye amemulika mahitaji ya kibinadamu..

“ Zaidi ya watu milioni 2.7 wanahitaji msaada, huku watu 450,000 wakiwa ni wakimbizi, na karibi raia 400,000 wa Car ni wakimbizi wa ndani. Hata hivyo, ni asilimia 30 tu ya mahitaji ya ufadhili yanayotimizwa. Nasizihi nchi wanachama kuendelea kusaidia maendeleo nchini humo kwa kufadhili mahitaji ya kibinadamu.”

Halikadhalika, ameeleza kwamba utaratibu wa mpito umehairishwa hadi mwisho wa mwaka huu, uchaguzi wa rais ukitarajiwa kufanyika mwezi Oktoba na Novemba, akisisitiza kwamba CAR iko kwenye njia panda na inahitaji msaada wa jamii ya kimataifa.