Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wahanga wa kiraia Afghanistan imeendelea kupanda- UNAMA

Idadi ya wahanga wa kiraia Afghanistan imeendelea kupanda- UNAMA

Takriban raia 5,000 wa Afghanistan wameuawa au kujeruhiwa kutokana na machafuko yanayoendelea nchini mwao katika miezi sita ya kwanza mwaka huu, kulingana na ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa ripoti ya kati ya mwaka iliyoandaliwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA, kumekuwa na vifo 1,592 na majeruhi 3,329 katika miezi sita ya kwanza. Nicholas Haysom ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu nchini Afghanistan na Mkuu wa UNAMA.

"Ripoti imebainisha kwamba takwimu za kati ya mwaka ikilinganishwa na wakati kama huu mwaka jana ni sawa. Tofauti iliyopo ni ndogo, kwani imeongezeka kwa asilimia nusu, lakini kinachoibuka ni idadi kubwa ya wahanga wa kiraia na kuangamizwa kwa maisha na mali ya raia."

Asilimia 90 ya raia waliofariki dunia waliuawa kwa mapigano ya ardhi, vilipuzi, mashambulizi ya kujitoa mhanga na mauaji ya kulenga moja kwa moja.