Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha mpango wa Obama kuhusu nishati safi

Ban akaribisha mpango wa Obama kuhusu nishati safi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha mpango kabambe wa Rais Obama kuhusu nishati isiyochafua mazingira, akiutaja kama uamuzi wa Marekani wa kukabiliana na ongezeko la joto duniani, kupunguza ubadhirifu na kukuza uchumi.

Akiongea na waandishi wa habari kuhusu mpango huo, msemaji wa Katibu Mkuu, Stephane Dujarric amesema

“Unatambua pia wajibu wetu wa kuviachia vizazi vijavyo sayari inayotoa fursa za maendeleo endelevu. Mpango huo ni mfano wa uongozi wa busara unaohitajika katika kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.”

Amesema Katibu Mkuu amefurahia uongozi wa Rais Obama ulio thabiti kuhusu mabadiliko ya tabianchi, na kwamba uongozi wake huo wa mfano ni muhimu katika kuzishawishi nchi nyingine kuungana ili kupitisha mkataba wa kudumu, unaowakilisha wote, na wenye maana mjini Paris, mwezi Disemba.