Mafuriko yameua watu 39 na kuathiri zaidi ya 200,000 Myanmar- OCHA

4 Agosti 2015

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA, imesema kuwa serikali ya Myanmar imeripoti kuuawa kwa watu 39, huku wengine 200,000 wakiathiriwa na mvua nzito na mafuriko nchini humo.

OCHA imesema takwimu hizo huenda zikaongezeka katika siku zijazo, wakati maeneo zaidi yakiweza kufikiwa na habari zaidi kupatikana.

Tathmini ya awali imeonyesha kuwa waathiriwa wanahitaji kwa dharura chakula, makazi, maji na huduma za kujisafi, pamoja na huduma za dharura za afya.

Jens Laerke ni msemaji wa OCHA, Geneva..

“Katika maeneo yaliyoathiriwa, mifumo ya usafiri, mitando ya nguvu za umeme na miundombinu ya mawasiliano imevurugwa, na kufikia maeneo mengi ni changamoto kubwa. Kwa mfano, uchafu mwingi unaoelea mitoni unatatiza kuwafikia watu walioathiriwa kwa boti, na barabara nyingi zimefungwa kwa maporomoko ya udongo.”

Bwana Laerke amesema mamlaka za Myanmar leo zimeomba rasmi usaidizi wa kimataifa, ingawa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa ya kibinadamu tayari yamekuwa yakishirikiana kwa karibu na mamlaka za Myanmar katika kusaidia jitihada za kutoa misaada tangu mafuriko yaanze mnamo Julai 30.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter