Ofisi ya Haki za binadamu yalaani mashambulizi Burundi
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, leo imelaani mashambulizi dhidi ya mtetezi wa haki za binadamu na mwandishi wa habari nchini Burundi, ikitoa wito kwa mamlaka za Burundi zichunguze matukio hayo mara moja.
Pierre Claver Mbonhimpa, mwanaharakati maarufu wa haki za binadamu, alijeruhiwa vibaya baada kufyatuliwa risasi mara nne na watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki hapo jana Agosti tatu, akiwa anaelekea nyumbani.
Mnamo Agosti pili, Esdras Ndikumana, mwandishi habari wa RFI na AFP alikamatwa kikatili na kuteswa na mawakala wa shirika la kitaifa la kijasusi, SNR, wakati akipiga picha kwenye eneo la tukio alikouliwa Jenerali Adolphe Nshimirimana.
“Tunatoa wito kwa mamlaka za Burundi zianzishe kasi uchunguzi ulio wazi na wa kina katika matukio haya, na kuhakikisha kuwa wahusika wanawajibishwa kisheria. Ukwepaji sheria kwa wakiukaji wa haki za binadamu ni lazima ukome. Tunalaani pia mauaji ya Jenerali Nshimirimana na kutaka wahalifu wakabiliwe kisheria.”
Ofisi hiyo pia imeeleza kutiwa wasiwasi na idadi kubwa ya watu ambao wamekuwa wakikamatwa kiholela nchini Burundi katika miezi michache iliyopita.