Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu alaani mauaji ya mlinda amani wa MINUSCA

Katibu Mkuu alaani mauaji ya mlinda amani wa MINUSCA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amelaani kuuawa kwa mlinda amani wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuimarisha hali nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA mjini Bangui.

Walinda amani wa MINUSCA walishambuliwa mnamo Agosti pili na kundi lenye silaha wakati wa operesheni ya kumsaka mshukiwa wa uhalifu, kufuatia kibali kilichotolewa na mwendesha mashtaka mkuu wa umma mjini Bangui. Washukiwa watatu walikamatwa na MINUSCA katika operesheni hiyo.

Akukutana na waandishi wa habari, Bwana Dujarric amesema:

“Mlinda amani mmoja aliuawa na wanane wengine kujeruhiwa, na MINUSCA imesema leo kuwa wote wanane hao wanaendelea vizuri na matibabu. Katibu Mkuu analaani vikali mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa, na kutoa wito hatua zichukuliwe kasi kuwafikisha washukiwa wa uhalifu huu mbele ya sheria.”

Ban ametoa wito pia kwa makundi yaliyojihami yaheshimu hadhi ya MINUSCA ya kutoegemea upande wowote, na kukaariri ahadi ya Umoja wa Mataifa kusaidia mamlaka za CAR katika kupambana na uhalifu na kutokomeza ukwepaji sheria, kulingana na mamlaka ya MINUSCA.