Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wawezeshe wanawake kukabiliana na ugaidi: UNAMI

Wawezeshe wanawake kukabiliana na ugaidi: UNAMI

Wanawake wanaweza kuwa nguzo muhimu katika kuleta mabadiliko na kushiriki katika juhudi bunifu za kuelimisha, pamoja na kutunga na kutekeleza sera na miradi ya kukabiliana na athari za mizozo, na kuenea kwa misimamo mikali na katili.

Hayo yamesemwa na Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, UNAMI, Gyorgy Busztin, wakati wa kufungua kongamano la kitaifa la siku mbili kuhusu kuwawezesha wanawake kukabiliana na athari za ugaidi.

Kongamano hilo ambalo limeandaliwa kwa pamoja na Umoja wa Mataifa, Wizara ya masuala ya wanawake nchini Iraq, na Baraza Kuu la Masuala ya Wanawake katika jimbo la Kurdistan, linamulika athari za misimamo mikali katili na ugaidi kwa wanawake na wasichana, hususan wale wanaotoka makundi ya walio wachache.

Linamulika pia ushiriki wa wanawake katika kuleta uuiano na maridhiano ya kijamii, na kufungua fursa za uwakilishi wa wanawake katika uongozi, kufanya maamuzi, na kutekeleza mikakati ya amani na usalama.