Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha kuafikiwa ajenda ya maendeleo baada ya 2015

Ban akaribisha kuafikiwa ajenda ya maendeleo baada ya 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha makubaliano yaliyoafikiwa na nchi wanachama wa Umoja huo kuhusu ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, ambayo itapitishwa kwenye mkutano wa wa Septemba 25 hadi 27, 2015. Taarifa kamili na Amina Hassan

(Taarifa ya Amina)

Ban amesema ajenda hiyo iitwayo: "kubadili dunia yetu: ajenda ya mwaka 2030 kwa maendeleo endelevu" inajumuisha masuala yanayowahusu wote, akiitaja kama ya kihistoria na inayowakilisha ufanisi mkubwa duniani.

Ban ameitaja pia ajenda hiyo kuwa ajenda ya wanadamu, ambayo ni mpango wa kutokomeza umaskini wa aina zote, bila kumwacha mtu yeyote nyuma. Amesema inalenga pia kuhakikisha amani na ufanisi, na kubuni ubia unaojali watu na sayari dunia.

Amesema malengo yote 17 ya maendeleo endelevu yaliyoafikiwa yanahusiana, na kwamba itaweka njia mpya ya kutokomeza umaskini, kugawana utajiri na kupambana na vichochea mabadiliko ya tabianchi.