Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asema UNMEER imetimiza lengo lake kuu, chanjo ya Ebola karibu

Ban asema UNMEER imetimiza lengo lake kuu, chanjo ya Ebola karibu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema kuwa wakati juhudi za kutokomeza Ebola zikiendelea Afrika Magharibi, hatua muhimu imepigwa kimataifa katika jitihada za kukabiliana na homa hiyo, leo ikiwa ni siku ya kufungwa kwa Ujumbe wa kukabiliana na dharura ya Ebola, UNMEER. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Bwana Ban amesema ujumbe wa UNMEER umetimiza lengo lake kuu la kuongeza kasi ya juhudi za kukabliana na mlipuko wa homa hiyo Afrika Magharibi, pamoja na kuleta pamoja wadau katika kusaidia juhudi za kitaifa katika nchi zilizoathiriwa.

Ban amesema ujumbe wa UNMEER unapofungwa leo Julai 31, majukumu ya kuratibu jitihada za kukabiliana na dharura ya Ebola zitahamishiwa kwa Shirika la Afya Duniani WHO kuanzia kesho Agosti mosi.

Wakati huo huo, Shirika la WHO limetangaza leo kuwa dunia ipo karibu kupata chanjo ifaayo kwa kuzuia maambukizi ya Ebola.

Matokeo ya tathmini ya awali ya awamu ya tatu ya majaribio ya chanjo aina ya VSV-EBOV nchini Guinea, yameonyesha kuwa chanjo hiyo ina uwezo mkubwa mno katika kuzuia kirusi cha Ebola, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Margaret Chan akisema inatia matumaini makubwa.