Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 100,000 kusajiliwa nchini Liberia: UNICEF

Watoto 100,000 kusajiliwa nchini Liberia: UNICEF

Nchini Liberia, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF linakadiria kwamba zaidi ya watoto 70,000 wako hatarani kutengwa iwapo hawatasajiliwa.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, UNICEF imesema kwamba idadi  ya watoto waliosajiliwa mwaka 2013 kabla ya mlipuko wa Ebola ilikuwa ni 79,000, idadi hiyo ikiwa ni 48,000 mwaka 2014 na 700 tu tangu mwanzo wa mwaka huu.

Akihojiwa na idhaa hii, Deirdra Kiernan, Kaimu Mwakilishi wa UNICEF nchini Liberia anaeleza kwanini usajili ulisuasua.

“ Kupunguka kwa kiwango cha usajili wa watoto kumetokea kwa sababu wakati wa mlipuko wa Ebola, vituo vya afya vilikuwa vimefungwa au havikufanya kazi ipasavyo, na watu walikuwa wanaogopa kupeleka watoto wachanga hospitalini,  wakiogopa kuambukizwa  Ebola” 

Ameeleza kwamba UNICEF pamoja  na serikali ya Liberia imezindua kampeni ya usajili wa watoto inayolenga kufikia watoto takribani  laki moja, akisisitiza changamoto zinazokumba mtoto  aiyesajiliwa.

“ Hatambuliki  , halindwi, sio raia  raia halali wa Liberia au nchi yoyote, akitaka kupata pasipoti au kusafiri, hawezi, kwa sababu hapewi  kitambulisho chochote, na ni hatari pia kwa serikali kutojua  raia ni wangapi na wako wapi, pia ni vigumu kupanga kwa mifumo ya afya na elimu, shule ngapi unahitaji na madarasa mangapi…”