Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjumbe wa UM alaani shambulio la uteketezaji Ukingo wa Magharibi, Gaza

Mjumbe wa UM alaani shambulio la uteketezaji Ukingo wa Magharibi, Gaza

Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani Mashariki ya Kati, Nickolay Mladenov, ameeleza kusikitishwa na shambulio la uteketezaji nyumba uliotekelezwa na watu wanaoshukiwa kuwa Wayahudi wenye msimamo mkali, na ambalo lilimuua mtoto mdogo wa Kipalestina aitwaye Ali. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Shambulio hilo lilofanyika katika kijiji cha Duma kwenye maeneo yalokaliwa Ukingo wa Magharibi, liliwajeruhi mamake na babake mtoto huyo vibaya, na pia kumjeruhi nduguye mwenye umri wa miaka minne.

Bwana Mladenov ametuma ujumbe wa kufariji kwa familia na rafiki za waathiriwa.

Aidha, ameunga mkono ujumbe wa kulaani vikali shambulio hilo, uliotolewa na serikali za Israel na Palestina, na kutoa wito uchunguzi wa kina ufanywe haraka ili kuwafikisha waliotenda uhalifu huo mbele ya mkono wa sheria.

Amesema mauaji hayo yalifanywa kwa misingi ya kisiasa, na kwamba vitendo kama hivyo visiruhusiwe kuibua chuki na ghasia na maafa zaidi, na pia kuvuruga matumaini ya amani.